2 Kwa hiyo, akamwambia, “Baba yangu anakusudia kukuua. Hivyo, jihadhari. Kesho asubuhi, jifiche mahali pa siri, ukae hapo.
3 Mimi nitakuja na kusimama karibu na baba yangu huko shambani mahali utakapokuwa. Hapo nitaongea naye juu yako, na kitu chochote nitakachogundua kutoka kwake, nitakueleza.”
4 Yonathani alimsifu Daudi mbele ya baba yake, akamwambia, “Usitende dhambi dhidi ya mtumishi wako Daudi kwani yeye hajatenda dhambi yoyote dhidi yako; matendo yake yote anapokutumikia daima yamekuwa mema kwako.
5 Alipomuua yule Mfilisti Goliathi, alihatarisha maisha yake, naye Mwenyezi-Mungu aliwapa Waisraeli ushindi mkubwa. Wewe ulipoona jambo lile ulifurahi. Kwa nini unataka kutenda dhambi kwa kumwaga damu isiyo na hatia kwa kumwua Daudi bila sababu?”
6 Shauli alimsikiliza Yonathani, kisha akaapa, “Naapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, sitamuua Daudi.”
7 Hivyo, Yonathani akamwita Daudi na kumweleza mambo hayo yote. Yonathani akampeleka Daudi kwa Shauli, na Daudi akamtumikia Shauli kama hapo awali.
8 Baadaye kulikuwa na vita tena kati ya Wafilisti na Waisraeli. Daudi alitoka akapigana na Wafilisti, akawaua Wafilisti wengi na waliosalia wakamkimbia.