4 Shauli aliposikia kwamba Daudi amekimbilia Gathi, hakumfuata tena.
5 Siku moja, Daudi akamwambia Akishi, “Kama nimepata kibali mbele yako nakuomba unipe mji mmoja nchini mwako ili uwe mahali pangu pa kuishi. Hakuna haja kwangu kuishi nawe katika mji huu wa kifalme.”
6 Siku hiyo, Akishi akampa mji wa Siklagi. Hivyo, tangu siku hiyo mji wa Siklagi umekuwa mali ya wafalme wa Yuda.
7 Daudi aliishi katika nchi ya Wafilisti kwa muda wa mwaka mmoja na miezi minne.
8 Katika muda huo, Daudi na watu wake waliwashambulia Wageshuri, Wagirizi na Waamaleki, ambao walikuwa wenyeji wa nchi hiyo tangu zamani. Aliwashambulia katika nchi yao mpaka Shuri, mpakani na Misri.
9 Daudi aliipiga nchi hiyo asimwache hai mtu yeyote, awe mwanamume au mwanamke, akateka kondoo, ng'ombe, punda, ngamia na mavazi; kisha akarudi na kufika kwa Akishi.
10 Akishi alipomwuliza, “Leo mashambulizi yako yalikuwa dhidi ya nani?” Daudi alimwambia, “Dhidi ya Negebu ya Yuda” au “Dhidi ya Negebu ya Wayerameeli” au “Dhidi ya Negebu ya Wakeni.”