17 Daudi aliwapiga tangu asubuhi hadi siku ya pili jioni. Hakuna mwanamume yeyote aliyenusurika isipokuwa vijana 400 ambao walipanda ngamia na kukimbia.
18 Daudi aliokoa kila kitu Waamaleki walichokuwa wamekiteka, hata na wake zake wawili.
19 Chochote kilichokuwa chao, kiwe kikubwa au kidogo, mtoto wa kiume au wa kike, Daudi alikikomboa.
20 Pia Daudi aliyarudisha makundi yote ya kondoo na ng'ombe, na watu wake wakawa wanaswaga wanyama hao wakiwatanguliza mbele ya wanyama wale wengine wakisema, “Nyara za Daudi.”
21 Daudi akawarudia wale watu 200 ambao waliachwa kwenye kijito cha Besori kwa sababu walikuwa wamechoka kumfuata. Wale watu walipomwona Daudi pamoja na wale waliokuwa pamoja naye, wakaenda kumlaki. Daudi alipofika karibu na watu hao, akawasalimu.
22 Lakini watu wote waovu na baradhuli miongoni mwa watu waliofuatana na Daudi, wakasema, “Hatutawapa watu hawa nyara zozote tulizozikomboa kwani hawakwenda pamoja nasi. Ila wawachukue wake zao na watoto wao, waende zao.”
23 Daudi akawaambia, “Sivyo ndugu zangu. Hamwezi kufanya hivyo kwa kile ambacho Mwenyezi-Mungu ametupa. Alitulinda salama, na akalitia mikononi mwetu genge lililokuja kutushambulia.