3 Daudi na watu wake walipofika mjini waliukuta mji umeteketezwa, na wanawake, watoto wao wa kiume na wa kike, wamechukuliwa mateka.
4 Ndipo Daudi na watu wake walipoangua kilio, wakalia hadi walipoishiwa nguvu.
5 Wake wawili wa Daudi, Ahinoamu kutoka Yezreeli na Abigaili mjane wa Nabali, nao pia walikuwa wamechukuliwa mateka.
6 Sasa, Daudi alikuwa katika matatizo makubwa kwa kuwa watu wake walikuwa na uchungu rohoni mwao kwa kupoteza watoto wao; hivyo wakawa wanamtishia kumpiga mawe. Lakini Daudi alijipa moyo kwa kumtegemea Mwenyezi-Mungu, Mungu wake.
7 Daudi akamwambia kuhani Abiathari mwana wa Ahimeleki, “Niletee kizibao cha kuhani.” Abiathari akampelekea.
8 Daudi akamwomba Mwenyezi-Mungu shauri, “Je, genge hili nilifuate? Na je nitalikamata?” Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Lifuate kwani utalipata na kuwaokoa hao waliotekwa.”
9 Kwa hiyo, Daudi akaondoka pamoja na wale watu 600 aliokuwa nao. Walipofika kwenye kijito cha Besori, wakawakuta baadhi ya watu waliotekwa wameachwa hapo.