3 Yoashi alikaa naye kwa muda wa miaka sita akiwa amefichwa ndani ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, wakati Athalia alipokuwa akitawala nchi.
4 Lakini katika mwaka wa saba Yehoyada alituma ujumbe na kuwakusanya makapteni wa Wakari na walinzi; akaamuru wamjie katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, naye akafanya nao mapatano na kuwaapisha humo katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Halafu akawaonesha Yoashi mwana wa mfalme Ahazia.
5 Kisha akatoa amri: “Mtafanya hivi: Mtakapokuja kushika zamu siku ya Sabato, theluthi moja italinda ikulu;
6 theluthi nyingine ikiwa kwenye lango la Suri na theluthi nyingine ikiwa kwenye lango nyuma ya walinzi. Hivyo ndivyo mtakavyolinda ikulu ili isivunjwe.
7 Yale makundi mawili ambayo humaliza zamu yao siku ya Sabato yatashika zamu katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu kumlinda mfalme.
8 Mtamzunguka mfalme, kila mtu na silaha yake mkononi na mtu yeyote atakayethubutu kuwakaribia lazima auawe. Lazima mkae na mfalme, awe anatoka au anakaa.”
9 Makapteni walitii amri zote alizotoa kuhani Yehoyada. Kila ofisa akawachukua watu wake wote, wale waliokuwa wamemaliza zamu na wale waliokuwa wanaingia kushika zamu siku ya Sabato, basi wakamwendea kuhani Yehoyada.