10 Shalumu mwana wa Yabeshi alikula njama dhidi ya mfalme Zekaria, akampiga mbele ya watu na kumwua, kisha akatawala mahali pake.
11 Matendo mengine yote ya Zekaria yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Israeli.
12 Basi tukio hilo lilitokana na ahadi ya Mwenyezi-Mungu kwa mfalme Yehu, kusema, “Wazawa wako watatawala Israeli mpaka kizazi cha nne.”
13 Katika mwaka wa thelathini na tisa wa enzi ya mfalme Azaria wa Yuda, Shalumu mwana wa Yabeshi alianza kutawala Israeli, akatawala huko Samaria kwa muda wa mwezi mmoja.
14 Menahemu mwana wa Gadi aliondoka Tirza kwenda Samaria, na huko akamuua Shalumu mwana wa Yabeshi, kisha akatawala mahali pake.
15 Matendo mengine yote ya Shalumu na njama zake zote alizofanya, yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Israeli.
16 Menahemu alipokuwa njiani kutoka Tirza, aliuharibu kabisa mji wa Tapua na kuangamiza wakazi wake pamoja na nchi yote iliyozunguka kwa sababu hawakujisalimisha kwake. Isitoshe, aliwatumbua wanawake waja wazito wote.