10 “Mwambieni Hezekia mfalme wa Yuda, ‘Usikubali Mungu wako unayemtegemea akudanganye kwa kukuahidi kwamba mji wa Yerusalemu hautatekwa na mfalme wa Ashuru.
11 Wewe umekwisha sikia jinsi wafalme wa Ashuru walivyozitenda nchi nyingine na kuziangamiza kabisa. Je, wadhani wewe utaokoka?
12 Je, miungu ya mataifa iliokoa Gozani, Harani, na Resefu na Waedeni waliokaa Telasari, mataifa ambayo babu zangu waliyaangamiza?
13 Wako wapi wafalme wa Hamathi, Arpadi, Sefarvaimu, Hena na wa Iva?’”
14 Mfalme Hezekia alipokea barua kutoka kwa wajumbe na kuisoma. Kisha akaenda na kuingia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, naye akaiweka mbele yake Mwenyezi-Mungu.
15 Halafu akamwomba Mwenyezi-Mungu akisema, “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, unayekaa katika kiti cha enzi juu ya viumbe wenye mabawa, ni wewe tu uliye Mungu, unayetawala falme zote za ulimwengu. Wewe uliumba nchi na mbingu.
16 Ee Mwenyezi-Mungu, fumbua macho uone, tega sikio lako, uyasikie matusi yote ambayo Senakeribu amepeleka kukutukana wewe Mungu uliye hai.