2 Aliwaamuru Eliakimu, mkuu wa ikulu, Shebna, katibu, na wazee wa makuhani, wamwendee nabii Isaya mwana wa Amozi, wakiwa wamevaa mavazi ya magunia.
3 Nao wakamwambia Isaya, “Hezekia anasema hivi, ‘Leo ni siku ya huzuni, siku ya kukemewa na ya dharau. Sisi tumekuwa kama mama ambaye anataka kujifungua mtoto, lakini hana nguvu ya kumzaa.
4 Inawezekana Mwenyezi-Mungu, Mungu wako alisikia maneno ya jemadari mkuu, ambaye ametumwa na mfalme wa Ashuru, bwana wake, ili kumtukana Mungu aliye hai; naye Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, atakaripia maneno aliyosikia. Kwa hiyo waombee watu waliobaki.’”
5 Basi, hao watumishi wa mfalme Hezekia walipokwisha fika kwa Isaya,
6 aliwaambia “Mwambieni bwana wenu kwamba Mwenyezi-Mungu asema hivi, ‘Usiogope kwa sababu ya maneno uliyoyasikia, ambayo watumishi wa mfalme wa Ashuru wameyasema kunikebehi.
7 Tazama nitamfanya mfalme asikie uvumi, halafu atarudi katika nchi yake na huko nitamfanya auawe kwa upanga.’”
8 Kisha yule jemadari mkuu aliposikia kwamba mfalme wa Ashuru alikuwa ameondoka Lakishi, aliondoka na kumkuta akiushambulia mji wa Libna.