5 Wanafunzi wa manabii huko Yeriko wakamwendea Elisha na kumwuliza, “Je, unajua kwamba hivi leo Mwenyezi-Mungu atamchukua bwana wako?” Elisha akawajibu, “Naam! Najua; nyamazeni.”
6 Kisha Elia akamwambia Elisha, “Tafadhali wewe kaa hapa; Mwenyezi-Mungu amenituma niende mtoni Yordani.” Lakini Elisha akasema, “Naapa kwamba kama Mwenyezi-Mungu aishivyo na kama wewe mwenyewe uishivyo sitakuacha.” Basi, wakaenda pamoja.
7 Manabii hamsini wakawafuata mpaka mtoni Yordani. Elia na Elisha wakasimama karibu na mto, nao manabii wakasimama mbali kidogo.
8 Elia akalivua vazi lake, akalikunja na kuyapiga maji, maji yakagawanyika katika sehemu mbili, nao wakavuka hadi ngambo ya pili, wakapitia mahali pakavu.
9 Walipofika ngambo, Elia akamwambia Elisha, “Niambie unalotaka nikufanyie kabla sijaondolewa kwako.” Elisha akamwambia, “Naomba sehemu maradufu ya roho yako.”
10 Elia akajibu, “Ombi lako ni gumu, hata hivyo utakipokea kipawa changu hicho ikiwa utaniona wakati nitakapoondolewa kwako; lakini usiponiona, basi hutapewa.”
11 Walipokuwa wanatembea na kuongea, ghafla, gari la moto likatokea pamoja na farasi wa moto; likawatenganisha; naye Elia akachukuliwa mbinguni katika kisulisuli.