8 Elia akalivua vazi lake, akalikunja na kuyapiga maji, maji yakagawanyika katika sehemu mbili, nao wakavuka hadi ngambo ya pili, wakapitia mahali pakavu.
9 Walipofika ngambo, Elia akamwambia Elisha, “Niambie unalotaka nikufanyie kabla sijaondolewa kwako.” Elisha akamwambia, “Naomba sehemu maradufu ya roho yako.”
10 Elia akajibu, “Ombi lako ni gumu, hata hivyo utakipokea kipawa changu hicho ikiwa utaniona wakati nitakapoondolewa kwako; lakini usiponiona, basi hutapewa.”
11 Walipokuwa wanatembea na kuongea, ghafla, gari la moto likatokea pamoja na farasi wa moto; likawatenganisha; naye Elia akachukuliwa mbinguni katika kisulisuli.
12 Elisha alipoona tukio hilo akalia, “Baba yangu, baba yangu! Gari la Israeli na wapandafarasi wake!” Basi, Elisha hakumwona tena Elia.Ndipo Elisha alipoyashika mavazi yake na kuyararua vipande viwili.
13 Kisha akaliokota vazi la Elia lililomwangukia, akarudi na kusimama ukingoni mwa mto Yordani.
14 Akayapiga maji kwa vazi la Elia akisema, “Yuko wapi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Elia?” Alipoyapiga maji, yakagawanyika sehemu mbili, naye akavuka hadi ngambo.