12 Wakati huo, mfalme Merodak-baladani mwana wa Baladani mfalme wa Babuloni alisikia kuwa Hezekia alikuwa ameugua na sasa amepona, akamtumia ujumbe pamoja na zawadi.
13 Basi, Hezekia akawakaribisha na kuwaonesha mali yake: Nyumba yake ya hazina, fedha, dhahabu, viungo vya kukolezea chakula, mafuta ya thamani na nyumba ya vifaa vyake vyote vya kijeshi na vitu vyote vilivyokuwamo katika bohari zake. Hakukuwa chochote katika ikulu yake, au nchi yake ambacho hakuwaonesha.
14 Ndipo nabii Isaya alipomwendea mfalme Hezekia na kumwuliza, “Watu hawa wamesema nini? Na, wamekujia kutoka wapi?” Naye Hezekia akamjibu, “Wamenijia kutoka nchi ya mbali.”
15 Halafu akamwuliza, “Wameona nini katika ikulu yako?” Hezekia akamjibu, “Wameona yote yaliyomo katika ikulu yangu. Hakuna chochote katika bohari zangu ambacho sikuwaonesha.”
16 Ndipo Isaya akamwambia Hezekia, “Sikia neno la Mwenyezi-Mungu:
17 Tazama, siku zinakuja ambapo vyote vilivyomo nyumbani mwako na vitu vyote walivyokusanya baba zako mpaka wakati huu vitapelekwa mpaka Babuloni. Hakuna kitu chochote kitakachobaki; ndivyo asemavyo Mwenyezi-Mungu.
18 Tena baadhi ya watoto wako wa kiume watapelekwa mateka, nao watakuwa matowashi katika ikulu ya mfalme wa Babuloni.”