16 Misri haitakuwa tena na nguvu za kuweza kutegemewa na watu wa Israeli. Waisraeli watakumbuka jinsi walivyokosa kwa kutegemea nchi ya Misri. Waisraeli watatambua kuwa mimi ni Bwana Mwenyezi-Mungu.”
17 Siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, mwaka wa ishirini na saba tangu uhamisho wetu, neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia:
18 “Wewe mtu! Nebukadneza, mfalme wa Babuloni, alilipa jeshi lake jukumu gumu la kuishambulia Tiro. Vichwa vyote vya wanajeshi wake vilipata upara na mabega yote yalichubuka. Lakini yeye, wala jeshi lake, hawakuambulia chochote kutokana na uvamizi huo alioufanya dhidi ya Tiro.
19 Kwa hiyo, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitampa Nebukadneza mfalme wa Babuloni, nchi ya Misri. Ataipora mali yake yote, na kuchukua utajiri wa Misri kuwa ujira wa jeshi lake.
20 Nimempa nchi ya Misri kuwa ujira wa jasho lake kwa kuwa majeshi yake yalifanya kazi kwa ajili yangu. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.
21 Siku hiyo, nitawafanya Waisraeli wawe na nguvu na kukuwezesha wewe Ezekieli uongee miongoni mwao. Nao watapata kujua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.”