6 Hapo ndipo wakazi wote wa Misri watatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.“Waisraeli walikutegemea wewe ee Misri, lakini umekuwa dhaifu kama utete.
7 Walipokushika kwa mkono, ulivunjika na kutegua mabega yao. Walipokuegemea ulivunjika na kutetemesha viungo vyao.
8 Kwa hiyo, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitazusha upanga dhidi yako na kuwaua watu na wanyama wako wote.
9 Kwa sababu umesema kuwa mto Nili ni wako, kwamba ndiwe uliyeufanya, basi, nchi yako, Misri, itakuwa tupu na jangwa. Ndipo watu watatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.
10 Hakika nitakuadhibu wewe na mito yako; kwa hiyo nitaifanya nchi ya Misri kuwa jangwa na tupu toka Migdoli mpaka Syene hadi mipakani mwa Kushi.
11 Hakuna mtu wala mnyama atakayepita huko. Haitakaliwa kwa muda wa miaka arubaini.
12 Kati ya miji yote iliyoharibiwa, miji ya Misri itakuwa mitupu kwa miaka arubaini. Nitawatawanya Wamisri kati ya watu wa mataifa mengine na kuwasambaza katika nchi nyingine.