18 Nikimwambia mtu mwovu kwamba hakika atakufa, nawe humwonyi au kumwambia aache njia yake potovu ili kuyaokoa maisha yake, basi, mtu huyo mwovu atakufa kwa uovu wake; lakini damu yake nitakudai wewe.
19 Lakini, ukimwonya mtu huyo mwovu naye hauachi uovu wake au njia yake potovu, mtu huyo atakufa kwa uovu wake, lakini wewe utakuwa umeyaokoa maisha yako.
20 Tena, kama mtu mwadilifu anauacha uadilifu wake na kutenda uovu, nami nikamwekea kikwazo, mtu huyo atakufa. Kwa vile hukumwonya, atakufa kwa sababu ya dhambi yake, nayo matendo yake ya uadilifu hayatakumbukwa. Lakini damu yake nitakudai wewe.
21 Lakini, ukimwonya mtu mwadilifu asitende dhambi, naye akaacha kutenda dhambi, hakika mtu huyo ataishi, kwa kuwa amepokea maonyo yako, nawe utakuwa umeyaokoa maisha yako.”
22 Nguvu ya Mwenyezi-Mungu ilikuwa juu yangu; naye akaniambia, “Inuka uende mpaka sehemu tambarare nami nitaongea nawe huko.”
23 Basi, nikainuka na kwenda sehemu tambarare. Lo! Nikiwa huko nikauona utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukiwa umesimama huko kama utukufu ule niliokuwa nimeuona karibu na mto Kebari; nami nikaanguka kifudifudi.
24 Lakini roho iliniingia na kunisimamisha wima. Kisha Mungu akaongea nami, akaniambia, “Nenda ukajifungie nyumbani mwako.