1 Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia:
2 “Wewe mtu! Mgeukie Gogu mfalme wa nchi ya Magogu ambaye ni mtawala mkuu wa Mesheki na Tubali.
3 Toa unabii juu yake na kumwambia kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Mimi nitapambana nawe ewe Gogu mtawala wa Mesheki na Tubali.
4 Mimi nitakuzungusha na kukutia ndoana matayani mwako, na kukutoa nje wewe pamoja na jeshi lako lote: Farasi na wapandafarasi na kundi kubwa la watu wamevaa mavazi ya vita, ngao na vigao mikononi, wanapunga mapanga yao.
5 Wanajeshi kutoka Persia, Kushi na Puti wako pamoja nao; wote wana ngao na kofia za chuma.
6 Pia vikosi kutoka Gomeri, Beth-togarma, upande wa kaskazini kabisa, na majeshi yao yote pamoja na majeshi kutoka mataifa mengine, yako pamoja nawe.
7 Jitayarishe, ukae wewe mwenyewe na jeshi lako lote pamoja na wengine wote ulio nao, ukawalinde.