13 Watu wote nchini watashughulika kuwazika. Na hilo litakuwa jambo la kuwapatia sifa, siku ile nitakapodhihirisha utukufu wangu. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.
14 Baada ya miezi hiyo saba, watachagua watu wapitepite nchini kutafuta maiti ambazo zitakuwa bado hazijazikwa, wazizike ili kuisafisha nchi.
15 Wakati wanapopitapita humo nchini, kama wakiona mfupa wa binadamu wataweka alama ili wale wanaozika waje na kuuzika katika Bonde la Hamon-gogu.
16 Huko kutakuwa pia mji utakaoitwa Hamona. Ndivyo watakavyoisafisha nchi.
17 “Sasa, ewe mtu, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Waite ndege wote na wanyama wote wa porini wakusanyike toka pande zote na kuja kula karamu ya kafara ninayowaandalia, ambayo itakuwa kubwa sana juu ya milima ya Israeli, ambako watakula nyama na kunywa damu.
18 Watakula nyama ya mashujaa, watakunywa damu ya wakuu wa dunia watakaochinjwa kama kondoo madume au wanakondoo, mbuzi au mafahali wanono wa Bashani.
19 Katika karamu hiyo ninayowafanyia watakula mafuta na kushiba. Watakunywa damu na kulewa.