7 Nitalifanya jina langu takatifu litambuliwe na watu wangu Israeli, wala sitaruhusu tena watu walikufuru jina langu takatifu. Nayo mataifa yatatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu, Mtakatifu wa Israeli.
8 “Siku ile ninayosema juu yake kwa hakika inakuja. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.
9 Hapo, watu waishio katika miji ya Israeli watatoka na kukusanya silaha zilizoachwa na kuzichoma moto. Watatumia hizo ngao, pinde, mishale, mikuki na marungu, kama kuni za kuwasha moto kwa muda wa miaka saba.
10 Hawatahitaji kuokota kuni mashambani, wala kukata miti msituni, kwani watazitumia hizo silaha kuwashia nazo moto. Watapora mali za wale waliopora mali zao na kuwapokonya wale waliopokonya mali zao. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.
11 “Katika siku ile, nitampa Gogu mahali pa kuzikwa katika nchi ya Israeli, katika Bonde la Wasafiri, upande wa mashariki wa bahari ya Chumvi. Gogu atazikwa huko pamoja na jeshi lake lote, nao wasafiri watazuiwa kupita huko. Bonde hilo litaitwa, ‘Bonde la Hamon-gogu’.
12 Kwa kuisafisha nchi Waisraeli watatumia muda wa miezi saba kuzika maiti hizo.
13 Watu wote nchini watashughulika kuwazika. Na hilo litakuwa jambo la kuwapatia sifa, siku ile nitakapodhihirisha utukufu wangu. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.