20 Utatwaa damu yake na kuitia juu ya pembe nne za madhabahu na juu ya ncha nne za daraja na juu ya pambizo yake pande zote. Hivyo ndivyo utakavyoitakasa madhabahu na kuiweka wakfu.
21 Utachukua pia fahali wa sadaka ya kuondoa dhambi; watamteketeza katika mahali palipochaguliwa ndani ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, lakini nje ya mahali patakatifu.
22 Kesho yake, utatoa beberu asiye na dosari, kuwa sadaka ya kuondoa dhambi; madhabahu itatakaswa kama ilivyotakaswa kwa damu ya fahali.
23 Utakapokwisha kuitakasa, utatwaa fahali mdogo asiye na dosari na kondoo dume mmoja asiye na dosari na
24 kuwaleta mbele yangu. Makuhani watawapaka chumvi na kuwatoa kuwa tambiko ya kuteketezwa, kwa Mwenyezi-Mungu.
25 Kwa muda wa siku saba, kila siku utatambika beberu mmoja awe sadaka ya kuondoa dhambi. Pia watatoa fahali mmoja na kondoo dume mmoja asiye na dosari.
26 Hivyo kwa muda wa siku saba, utafanya upatanisho na kuitakasa, na hivyo kuiweka wakfu madhabahu.