19 Hatutamiliki mali yoyote miongoni mwao ngambo ya mto Yordani, kwa sababu sisi tumepata maeneo yetu ngambo hii, mashariki ya mto Yordani.”
20 Mose akawaambia, “Kama kweli mtafanya kama mlivyosema, basi papa hapa mbele ya Mwenyezi-Mungu, chukueni silaha zenu kwenda vitani.
21 Kila mpiganaji wenu atavuka mto Yordani na mkiwa chini ya uongozi wa Mwenyezi-Mungu, mtawashambulia adui zetu mpaka Mwenyezi-Mungu awashinde,
22 na kuimiliki nchi. Mkisha fanya hayo, mtarudi, maana mtakuwa mmetimiza wajibu wenu kwa Mwenyezi-Mungu na ndugu zenu Waisraeli. Kisha Mwenyezi-Mungu atakubali nchi hii ya mashariki ya Yordani kuwa mali yenu.
23 Lakini nawaonyeni kwamba msipotimiza ahadi yenu, mtakuwa mnamtendea Mwenyezi-Mungu dhambi; jueni kwa hakika kwamba mtaadhibiwa.
24 Wajengeeni watoto wenu miji na kondoo wenu mazizi; lakini fanyeni kama mlivyoahidi.”
25 Kisha, watu wa Gadi na wa Reubeni wakamwambia Mose, “Sisi watumishi wako tutafanya kama ulivyotuamuru.