21 Kila mpiganaji wenu atavuka mto Yordani na mkiwa chini ya uongozi wa Mwenyezi-Mungu, mtawashambulia adui zetu mpaka Mwenyezi-Mungu awashinde,
22 na kuimiliki nchi. Mkisha fanya hayo, mtarudi, maana mtakuwa mmetimiza wajibu wenu kwa Mwenyezi-Mungu na ndugu zenu Waisraeli. Kisha Mwenyezi-Mungu atakubali nchi hii ya mashariki ya Yordani kuwa mali yenu.
23 Lakini nawaonyeni kwamba msipotimiza ahadi yenu, mtakuwa mnamtendea Mwenyezi-Mungu dhambi; jueni kwa hakika kwamba mtaadhibiwa.
24 Wajengeeni watoto wenu miji na kondoo wenu mazizi; lakini fanyeni kama mlivyoahidi.”
25 Kisha, watu wa Gadi na wa Reubeni wakamwambia Mose, “Sisi watumishi wako tutafanya kama ulivyotuamuru.
26 Wake zetu, watoto wetu na kondoo na ng'ombe, watabaki hapa katika miji ya Gileadi.
27 Lakini sisi watumishi wako tuko tayari kwenda vitani chini ya uongozi wa Mwenyezi-Mungu. Tutavuka mto Yordani na kupigana, kama ulivyosema.”