23 Lakini nawaonyeni kwamba msipotimiza ahadi yenu, mtakuwa mnamtendea Mwenyezi-Mungu dhambi; jueni kwa hakika kwamba mtaadhibiwa.
24 Wajengeeni watoto wenu miji na kondoo wenu mazizi; lakini fanyeni kama mlivyoahidi.”
25 Kisha, watu wa Gadi na wa Reubeni wakamwambia Mose, “Sisi watumishi wako tutafanya kama ulivyotuamuru.
26 Wake zetu, watoto wetu na kondoo na ng'ombe, watabaki hapa katika miji ya Gileadi.
27 Lakini sisi watumishi wako tuko tayari kwenda vitani chini ya uongozi wa Mwenyezi-Mungu. Tutavuka mto Yordani na kupigana, kama ulivyosema.”
28 Basi, Mose akatoa amri zifuatazo kwa kuhani Eleazari, kwa Yoshua mwana wa Nuni, na kwa viongozi wa jamaa za makabila ya Waisraeli:
29 “Ikiwa watu wa Gadi na wa Reubeni watavuka mto Yordani pamoja nanyi wakiwa na silaha zao chini ya uongozi wa Mwenyezi-Mungu, mkashinda na kuichukua nchi hiyo, basi mtawapa nchi ya Gileadi iwe mali yao.