20 Lakini wazawa wa Kohathi hawataingia kamwe kuvitazama vitu hivyo vitakatifu sana; wakifanya hivyo watakufa.”
21 Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose,
22 “Wahesabu watu wa ukoo wa Gershoni, kufuatana na familia na koo zao;
23 utawahesabu wanaume wote wenye umri kati ya miaka thelathini na hamsini wanaofaa kujiunga na huduma ya hema la mkutano.
24 Wajibu wao utakuwa huu: Watabeba mapazia ya hema takatifu na hema la mkutano pamoja na
25 kifuniko chake, kifuniko cha ngozi laini ya mbuzi kilicho juu yake, pazia la lango,
26 mapazia na kamba za ua ulio kandokando ya hema na madhabahu, mapazia ya lango la kitalu, na vifaa vyote vinavyotumika pamoja na vitu hivi. Wao watashughulika na mambo yote yanayohusika na vitu hivi.