13 akalala na mtu mwingine bila ya mumewe au mtu mwingine yeyote kujua; amejitia najisi lakini hakuna mtu aliyeshuhudia kitendo chake kwa kuwa hakufumaniwa.
14 Basi, mumewe akiingiwa na shaka na kuwa na wivu juu ya mkewe aliyejitia najisi; au kama amekuwa na wivu juu ya mke wake ingawa mkewe hakujitia najisi,
15 basi wote wawili watakwenda kwa kuhani na kupeleka sadaka inayotakiwa, yaani sehemu ya kumi ya unga wa shayiri; lakini bila kuitia mafuta au ubani, kwa kuwa ni sadaka ya nafaka ya mume anayemshuku mkewe, sadaka inayotolewa kuhusu kosa ambalo linabainishwa.
16 “Kuhani atampeleka huyo mwanamke karibu, na kumsimamisha mbele ya Mwenyezi-Mungu.
17 Kisha, atamimina maji matakatifu katika chombo cha udongo na kutwaa vumbi kutoka sakafuni mwa hema takatifu na kuitia katika maji hayo ili kuyafanya machungu.
18 Kuhani atamweka mbele ya Mwenyezi-Mungu na kumfunua nywele na kumpa sadaka hiyo ya nafaka itolewayo kwa sababu ya shuku ya mumewe. Kuhani mwenyewe atashikilia kile chombo chenye maji machungu yaletayo laana.
19 Halafu kuhani atamwapisha mwanamke huyo akisema: ‘Ikiwa hukulala na mwanamume mwingine, ukajitia najisi hali uko chini ya mamlaka ya mumeo, basi, hutapatwa na laana iletwayo na maji haya machungu.