1 Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose,
2 “Wape Waisraeli maagizo yafuatayo: Iwapo mwanamume au mwanamke ataweka nadhiri maalumu, nadhiri ya kujiweka wakfu, akajitenga kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu,
3 basi, asinywe divai au kileo, asinywe siki ya divai au ya namna nyingine, asinywe maji ya zabibu wala kula zabibu zilizoiva au kavu.
4 Muda wote atakaokuwa mnadhiri asile kitu chochote kinachotokana na mzabibu, tangu kokwa hata maganda yake.
5 “Siku zote za nadhiri yake ya kujitenga, hatanyoa nywele zake; mpaka muda wa nadhiri yake ya kujiweka wakfu kwa Mwenyezi-Mungu utakapomalizika, atakuwa mtakatifu, ataziacha nywele zake ziwe ndefu.