1 Siku Mose alipomaliza kulisimamisha hema takatifu, kulimiminia mafuta na kuliweka wakfu pamoja na vyombo vyake vyote, kuimiminia mafuta na kuiweka wakfu madhabahu na vyombo vyake vyote,
2 viongozi wa Israeli na wakuu wa koo na viongozi wa makabila ambao walisimamia watu wale waliohesabiwa,
3 walimletea Mwenyezi-Mungu matoleo yao: Magari yaliyofunikwa sita na mafahali kumi na wawili, gari moja kwa kila viongozi wawili na fahali mmoja kwa kila kiongozi. Baada ya kuvitoa mbele ya hema takatifu,
4 Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose,
5 “Pokea matoleo haya ili yatumiwe katika huduma itakayofanywa kwa ajili ya hema la mkutano, uwape Walawi, kila mmoja kwa kadiri ya kazi yake.”
6 Basi, Mose akachukua magari na mafahali akawapa Walawi.
7 Wagershoni wakapewa magari mawili na mafahali wanne, kwa kadiri ya huduma yao,