15 Baada ya kuwatakasa Walawi na kuwatoa kama sadaka ya kutikiswa wataingia ili kuhudumu katika hema la mkutano.
16 Hao wametolewa wawe wangu kabisa, badala ya wazaliwa wa kwanza wa Waisraeli.
17 Maana wazaliwa wote wa kwanza miongoni mwa Waisraeli ni wangu, wanadamu na wanyama; kwa sababu katika siku nilipowaua wazaliwa wote wa kwanza nchini Misri, niliwaweka wakfu kwangu.
18 Sasa ninawachukua Walawi badala ya wazaliwa wa kwanza wa Waisraeli,
19 na nimempa hao Aroni na wanawe, kama zawadi kutoka kwa Waisraeli, ili wafanye kazi katika hema la mkutano kwa ajili ya Waisraeli na kuwafanyia upatanisho ili pasitokee pigo miongoni mwa Waisraeli wakikaribia mahali patakatifu.”
20 Kwa hiyo Mose, Aroni na jumuiya yote ya Waisraeli wakawaweka wakfu Walawi, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose.
21 Walawi wakajitakasa dhambi na kuzifua nguo zao, naye Aroni akawatoa kama sadaka ya kutikiswa mbele ya Mwenyezi-Mungu. Pia, Aroni alifanya upatanisho kwa ajili yao ili kuwatakasa.