20 Kwa hiyo Mose, Aroni na jumuiya yote ya Waisraeli wakawaweka wakfu Walawi, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose.
21 Walawi wakajitakasa dhambi na kuzifua nguo zao, naye Aroni akawatoa kama sadaka ya kutikiswa mbele ya Mwenyezi-Mungu. Pia, Aroni alifanya upatanisho kwa ajili yao ili kuwatakasa.
22 Baada ya hayo Walawi waliingia na kufanya huduma yao katika hema la mkutano chini ya usimamizi wa Aroni na wanawe, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose.
23 Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose,
24 “Kila Mlawi mwenye umri wa miaka ishirini na mitano na zaidi, atahudumu katika hema langu la mkutano;
25 na kustaafu afikishapo umri wa miaka hamsini.
26 Baada ya hapo, anaweza kuwasaidia Walawi wenzake wanapohudumu katika hema, lakini haruhusiwi kutoa huduma yoyote peke yake. Ndivyo utakavyowapangia kazi Walawi.”