Hosea 9 BHN

Hosea anatangaza adhabu ya Israeli

1 Msifurahi enyi Waisraeli!Msifanye sherehe kama mataifa mengine;maana, mmekuwa wazinzi kwa kumwacha Mungu wenu.Mmefurahia malipo ya uzinzi,kila mahali pa kupuria nafaka.

2 Lakini ngano na mapipa ya divai haitawalisha,hamtapata divai mpya.

3 Hawatakaa katika nchi ya Mwenyezi-Mungu;naam, watu wa Efraimu watarudi utumwani Misri;watakula vyakula najisi huko Ashuru.

4 Hawatamtolea Mwenyezi-Mungu sadaka ya divai,wala hawatamfurahisha kwa tambiko zao.Chakula chao kitakuwa kama cha matanga,wote watakaokila watatiwa unajisi.Kitakuwa chakula cha kuwashibisha tu,hakitafaa kuletwa nyumbani kwa Mwenyezi-Mungu.

5 Mtafanya nini katika sikukuu ile iliyopangwa,au katika karamu ya Mwenyezi-Mungu?

6 Mtakapoyakimbia maangamizi ya nchi yenu,Misri itawakaribisheni kwake,lakini makaburi yenu yawangoja huko Memfisi.Magugu yatamiliki hazina zenu za fedha,miiba itajaa katika mahema yenu.

7 Siku za adhabu zimewadia,naam, siku za kulipiza kisasi zimefika;Waisraeli lazima wautambue wakati huo!Nyinyi mnasema, “Nabii ni mpumbavu;anayeongozwa na roho ni mwendawazimu.”Mnasema hivyo kwa sababu ya uovu wenu mkubwa,kwa sababu ya chuki yenu kali dhidi yake.

8 Nabii ni mlinzi wa Waefraimu kwa niaba ya Mungu;lakini, kokote aendako anategewa mtego kama ndege.Hata nyumbani mwa Mungu wake anachukiwa.

9 Nyinyi mmezama katika uovu,kama ilivyokuwa kule Gibea.Mungu atayakumbuka makosa yao,na kuwaadhibu kwa dhambi zao.

Dhambi ya Israeli na matokeo yake

10 Mwenyezi-Mungu asema:“Nilipowakuta Waisraeliwalikuwa kama zabibu jangwani.Nilipowaona wazee wenuwalikuwa bora kama tini za kwanza.Lakini mara walipofika huko Baal-peori,walijiweka wakfu kuabudu chukizo Baali,wakawa chukizo kama hicho walichokipenda.

11 Fahari ya Efraimu itatoweka kama ndege;watoto hawatazaliwa tena,hakutakuwa na watoto wa kuzaliwa,wala hakutakuwa na kuchukuliwa mimba!

12 Hata kama wakilea watoto,sitamwacha hai hata mmoja wao.Ole wao, nitakapowaacha peke yao!”

13 Kama nilivyokwisha ona hapo kwanza,Efraimu alikuwa kama mtende mchanga penye konde zuri;lakini sasa Efraimu itamlazimu kuwapeleka watoto wake wauawe.

14 Uwaadhibu watu hawa ee Mwenyezi-Mungu!Lakini utawaadhibu namna gani?Uwafanye wanawake wao kuwa tasa;uwafanye wakose maziwa ya kunyonyesha watoto wao!

Hukumu ya Mwenyezi-Mungu kwa Israeli

15 Mwenyezi-Mungu asema hivi:“Uovu wao wote ulianzia Gilgali;huko ndiko nilipoanza kuwachukia.Kwa sababu ya uovu wa matendo yao,nitawafukuza nyumbani kwangu.Sitawapenda tena.Viongozi wao wote ni waasi.

16 Watu wa Efraimu wamepigwa,wamekuwa kama mti wenye mzizi mkavu,hawatazaa watoto wowote.Hata kama wakizaa watoto,nitawaua watoto wao wawapendao.”

17 Kwa vile wamekataa kumsikiliza,Mungu wangu atawatupa;wao watatangatanga kati ya mataifa.

Sura

1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13 14