Hosea 1 BHN

1 Neno la Bwana lililomjia Hosea mwana wa Beeri, nyakati za Uzia, Yothamu, Ahazi na Hezekia, wafalme wa Yuda, na Yeroboamu mwana wa Yoashi, mfalme wa Israeli.

Mke na watoto wa Hosea

2 Mwenyezi-Mungu alipoanza kuongea na Waisraeli kwa njia ya Hosea, alimwambia hivi: “Nenda ukaoe mwanamke mzinzi, uzae naye watoto wa uzinzi, maana watu wa nchi hii wanafanya uzinzi mwingi kwa kuniacha mimi.”

3 Basi, Hosea akaenda, akamwoa Gomeri, binti Diblaimu. Gomeri akapata mimba, akamzalia Hosea mtoto wa kiume.

4 Mwenyezi-Mungu akamwambia Hosea, “Mpe mtoto huyo jina ‘Yezreeli’, maana bado kitambo kidogo tu, nami nitaiadhibu jamaa ya Yehu kwa mauaji aliyoyafanya bondeni Yezreeli. Nitaufutilia mbali ufalme katika taifa la Israeli.

5 Siku hiyo, nitazivunja nguvu za kijeshi za Israeli huko bondeni Yezreeli.”

6 Gomeri alipata mimba tena, akazaa mtoto wa kike. Mwenyezi-Mungu akamwambia Hosea, “Mpe mtoto huyo jina ‘Asiyehurumiwa’, maana sitawahurumia tena Waisraeli wala sitawasamehe.

7 Lakini nitawahurumia watu wa Yuda na kuwaokoa. Mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, nitawaokoa, lakini si kwa nguvu za kijeshi, au pinde, au panga, au farasi au wapandafarasi.”

8 Gomeri alipomwachisha kunyonya “Asiyehurumiwa,” alipata mimba tena, akamzalia Hosea mtoto mwingine wa kiume.

9 Mwenyezi-Mungu akamwambia Hosea, “Mpe mtoto huyo jina ‘Siwangu,’ maana nyinyi si watu wangu, wala mimi si wenu.”

Hali ya Israeli itarekebishwa

10 Lakini idadi ya Waisraeli itakuwa kubwa kama mchanga wa pwani ambao haupimiki wala hauhesabiki. Pale ambapo Mungu aliwaambia, “Nyinyi si watu wangu,” sasa atawaambia, “Nyinyi ni watoto wa Mungu aliye hai.”

11 Watu wa Yuda na wa Israeli wataungana pamoja na kumchagua kiongozi wao mmoja; nao watastawi katika nchi yao. Hiyo itakuwa siku maarufu ya Yezreeli.

Sura

1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13 14