15 Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Kwa nini mnanililia? Waambie Waisraeli waendelee mbele.
16 Inua fimbo yako na kuinyosha juu ya bahari. Maji yatagawanyika na Waisraeli wataweza kuvuka katikati ya bahari mahali pakavu.
17 Mimi nitawafanya Wamisri kuwa wakaidi, nao watawafuatia katikati ya bahari; nami nitajipatia utukufu kutokana na kuangamizwa kwa Farao na jeshi lake, magari yake ya vita pamoja na wapandafarasi wake.
18 Naam, nitatukuka kwa kumwangamiza Farao na jeshi lake, pamoja na magari yake na wapandafarasi; nao Wamisri watajua kwamba mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.”
19 Basi, malaika wa Mungu aliyekuwa mbele ya kundi la Waisraeli aliondoka akakaa nyuma yao. Na ule mnara wa wingu pia uliondoka mbele ukasimama nyuma yao,
20 ukakaa katikati ya Waisraeli na Wamisri. Lile wingu likawatia Wamisri giza, lakini likawaangazia Waisraeli usiku. Kwa hiyo, makundi hayo mawili, jeshi la Farao na kundi la Waisraeli, hayakukaribiana usiku kucha.
21 Mose akaunyosha mkono wake juu ya bahari, naye Mwenyezi-Mungu akaisukuma bahari nyuma kwa upepo mkali toka mashariki. Upepo huo ulivuma usiku kucha, ukaigawa bahari sehemu mbili na katikati kukatokeza nchi kavu.