14 “Mara tatu kila mwaka mtafanya sikukuu kwa heshima yangu.
15 Mtaadhimisha sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu: Kama nilivyowaagiza, mtakula mikate isiyotiwa chachu kwa siku saba wakati uliopangwa katika mwezi wa Abibu, kwa sababu katika mwezi huo mlitoka Misri. Mtu yeyote asije mbele yangu mikono mitupu.
16 Mtaadhimisha sikukuu ya mavuno ya kwanza ya kazi zenu na ya mavuno ya mashamba yenu. Mtaadhimisha sikukuu ya kukusanya mavuno mwishoni mwa mwaka mnapokusanya mazao ya kazi zenu.
17 Mara tatu kwa mwaka wanaume wote watakusanyika mbele zangu mimi Bwana Mwenyezi-Mungu.
18 “Usinitolee damu ya tambiko yangu pamoja na mkate uliotiwa chachu, wala usiyaache mafuta ya sikukuu yangu yabaki mpaka asubuhi.
19 “Mazao ya kwanza ya ardhi yako utayaleta nyumbani kwangu mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako.“Usimchemshe mwanakondoo au mwanambuzi katika maziwa ya mama yake.
20 “Tazameni, mimi namtuma malaika awatangulie safarini ili awalinde na kuwafikisha katika nchi niliyowatayarishia.