6 Kisha utatengeneza kulabu hamsini za dhahabu ili kuunganishia vile vipande viwili vya mapazia, hivyo hema litakuwa kitu kimoja.
7 “Pia utatengeneza kifuniko cha hema kwa mapazia kumi na moja ya manyoya ya mbuzi.
8 Kila pazia litakuwa na urefu wa mita 13, na upana wa mita 2. Mapazia yote hayo 11 yatakuwa na kipimo kilekile.
9 Utaunga mapazia matano pamoja, na mapazia sita pamoja. Pazia la sita utalikunja mara mbili mbele ya hema.
10 Kisha utafanya vitanzi hamsini upindoni mwa pazia la mwisho la kipande cha kwanza, na vitanzi hamsini upindoni mwa pazia la mwisho la kipande cha pili.
11 Utatengeneza kulabu hamsini za shaba na kuziingiza katika vile vitanzi hamsini ili kuunganishia vile vipande viwili vya mapazia na hivyo kufanya pazia moja la hema.
12 Ile nusu ya pazia iliyobaki utaitundika upande wa nyuma wa hema.