16 Nawe utamchinja na damu yake utairashia madhabahu pande zake zote.
17 Halafu utamkata huyo kondoo vipandevipande; utaosha matumbo yake na miguu yake, uviweke vyote pamoja na kichwa na vipande vingine.
18 Kisha utamteketeza kondoo mzima juu ya madhabahu ili kunitolea sadaka ya kuteketezwa; harufu ya sadaka inayotolewa kwa moto itanipendeza mimi Mwenyezi-Mungu.
19 “Utamchukua yule kondoo mwingine, naye Aroni na wanawe wataweka mikono yao juu ya kichwa chake.
20 Nawe utamchinja na kuchukua kiasi cha damu na kumpaka Aroni na wanawe kwenye ncha za masikio yao ya kulia na vidole gumba vya mikono yao ya kulia, na vidole gumba vya miguu yao ya kulia. Damu inayobaki utairashia madhabahu pande zake zote.
21 Kisha utachukua kiasi cha damu iliyoko juu ya madhabahu pamoja na yale mafuta ya kupaka umnyunyizie Aroni na mavazi yake, uwanyunyizie pia wanawe na mavazi yao. Aroni na wanawe watakuwa wamewekwa wakfu kwangu pamoja na mavazi yao yote.
22 “Kisha utachukua mafuta ya huyo kondoo dume: Mkia wake, mafuta yanayofunika matumbo na sehemu bora ya maini, figo zake mbili na mafuta yake, pamoja na paja la kulia. (Kondoo huyo ni kondoo wa kuweka wakfu.)