37 Kwa siku saba utaifanyia madhabahu upatanisho na kuiweka wakfu. Baada ya hayo, madhabahu itakuwa takatifu kabisa na chochote kitakachoigusa kitakuwa kitakatifu.
38 “Kila siku, wakati wote ujao, utatolea sadaka juu ya madhabahu: Wanakondoo wawili wenye umri wa mwaka mmoja.
39 Mwanakondoo mmoja utamtoa sadaka asubuhi na mwingine jioni.
40 Pamoja na mwanakondoo wa kwanza, utatoa kilo moja ya unga laini uliochanganywa na lita moja ya mafuta safi, na lita moja ya divai kama sadaka ya kinywaji.
41 Hali kadhalika na yule mwanakondoo mwingine wa jioni utamtolea tambiko pamoja na sadaka ya nafaka na ya kinywaji kama ulivyofanya asubuhi; harufu ya tambiko hiyo inayotolewa kwa moto itanipendeza mimi Mwenyezi-Mungu.
42 Sadaka hii ya kuteketezwa itatolewa daima, kizazi hata kizazi, mbele yangu mimi Mwenyezi-Mungu, mbele ya mlango wa hema la mkutano ambapo mimi nitakutana nanyi na kuongea nanyi.
43 Hapo ndipo nitakapokutana na Waisraeli na utukufu wangu utapafanya pawe patakatifu.