13 Lakini mtazibomoa madhabahu zao na kuzivunja nguzo zao za ibada na sanamu zao za Ashera.
14 Msiabudu mungu yeyote mwingine, maana mimi Mwenyezi-Mungu najulikana kwa jina: ‘Mwenye Wivu,’ mimi ni Mungu mwenye wivu.
15 Msifanye mikataba yoyote na wakazi wa nchi hiyo, maana watakapoiabudu miungu yao ya uongo na kuitambikia, watawaalikeni, nanyi mtashawishiwa kula vyakula wanavyoitambikia miungu yao,
16 nao wavulana wenu wakaoa binti zao, na hao binti wanaoabudu miungu yao, wakawashawishi wavulana wenu kufuata miungu yao.
17 “Msijifanyie miungu ya uongo ya chuma.
18 “Mtaiadhimisha sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu. Kwa muda wa siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu wakati uliopangwa katika mwezi wa Abibu, kama nilivyowaamuru, kwa sababu katika mwezi huo wa Abibu mlitoka Misri.
19 Kila mzaliwa wa kwanza wa kiume ni wangu, pamoja na wazaliwa wa kwanza wa kiume wa wanyama wako wote, wa ng'ombe na wa kondoo.