28 Mose alikaa huko mlimani pamoja na Mwenyezi-Mungu siku arubaini, mchana na usiku; hakula chakula wala kunywa maji. Aliandika maneno yote ya agano na zile amri kumi.
29 Mose alipokuwa anashuka mlimani Sinai akiwa na vile vibao viwili vyenye maneno ya agano mikononi mwake, hakujua kuwa uso wake ulikuwa unangaa kwa sababu alikuwa ameongea na Mwenyezi-Mungu.
30 Aroni na watu Waisraeli wote walipomwona waliogopa kumkaribia, kwani uso wake ulikuwa unangaa.
31 Lakini Mose alimwita Aroni na viongozi wa jumuiya ya Waisraeli waende karibu naye, kisha akazungumza nao.
32 Baadaye Waisraeli wote wakaja karibu naye, naye akawapa amri zote ambazo Mwenyezi-Mungu alimpa kule mlimani Sinai.
33 Mose alipomaliza kuzungumza na watu aliufunika uso wake kwa kitambaa.
34 Lakini ikawa kwamba kila mara Mose alipokwenda kuongea na Mwenyezi-Mungu katika hema la mkutano, alikiondoa kile kitambaa mpaka alipotoka nje. Na alipotoka nje aliwaambia Waisraeli mambo yote aliyoamriwa,