16 Vyandarua vyote kuuzunguka ua vilikuwa vya kitani safi iliyosokotwa.
17 Vikalio vyote vya nguzo vilikuwa vya shaba, lakini kulabu za nguzo hizo na vitanzi vyake vilikuwa vya fedha. Matumba yake yalikuwa ya fedha; pia nguzo zake zote zilishikamanishwa kwa fito za fedha.
18 Pazia la mlango wa ua lilitengenezwa kwa sufu ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na kitani safi iliyosokotwa, na kutariziwa vizuri; nalo lilikuwa na urefu wa mita 9 na kimo cha mita 2, kulingana na vyandarua vya ua.
19 Pia nguzo zake zilikuwa nne na vikalio vinne vya shaba. Kulabu zake zilikuwa za fedha, hata nguzo zake na vitanzi vyake vilikuwa vya fedha.
20 Vigingi vyote vya hema na vya ua kandokando ya hema vilikuwa vya shaba.
21 Ifuatayo ni orodha ya vifaa vilivyotumika katika kulijenga hema takatifu, yaani hema la agano. Orodha hii ilitayarishwa na Walawi kwa amri ya Mose, chini ya uongozi wa Ithamari, mwana wa kuhani Aroni.
22 Bezaleli, mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila la Yuda, alifanya kila kitu ambacho Mwenyezi-Mungu alimwamuru Mose.