3 Loti akawasihi sana, mwishowe wakakubali, wakageuka na kuingia nyumbani kwake. Loti akawaandalia karamu, akaoka mikate isiyotiwa chachu, wakala.
4 Lakini kabla ya kulala usiku, wanaume wote wa mji wa Sodoma, vijana kwa wazee, bila kubaki hata mmoja, wakaizingira nyumba ya Loti.
5 Wakamwita Loti na kumwuliza, “Wako wapi wale wanaume waliokuja kwako? Watoe nje. Tunataka kulala nao.”
6 Loti akatoka nje, akafunga mlango nyuma yake,
7 akawaambia, “Ndugu zangu, nawasihi msitende uovu huo.
8 Tazama, ninao binti wawili ambao bado hawajalala na mwanamume. Mniruhusu niwapeni hao wasichana muwatendee kama mpendavyo. Lakini msiwatende lolote wanaume hawa kwa sababu ni wageni wangu.”
9 Lakini wao wakasema, “Tupishe! Wewe ulikuja huku ukiwa mgeni na sasa wajifanya hakimu! Basi, tutakutenda mabaya zaidi ya hao wageni wako.” Hapo wakamsukuma Loti nyuma hata karibu wauvunje mlango wake.