3 nami nitakuapisha kwa jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa mbingu na dunia, kwamba hutamwoza mwanangu msichana yeyote miongoni mwa binti za Wakanaani ninaoishi nao.
4 Niapie kwamba utakwenda mpaka katika nchi yangu, kwa jamaa zangu, umtafutie mwanangu Isaka mke.”
5 Mtumishi akamwambia, “Huenda mwanamke huyo atakataa kufuatana nami kuja huku, ikiwa hivyo, je, ni lazima nimrudishe mwanao nchini ulikotoka?”
6 Abrahamu akamwambia, “La! Angalia sana usimrudishe mwanangu huko.
7 Mwenyezi-Mungu, Mungu wa mbingu, aliyenitoa nyumbani kwa baba yangu na kutoka katika nchi nilimozaliwa, na ambaye alisema nami, aliniapia kwamba atawapa wazawa wangu nchi hii. Yeye atamtuma malaika wake mbele yako ili umletee mwanangu mke kutoka huko.
8 Iwapo mwanamke huyo hatapenda kufuatana nawe hadi huku, basi kiapo changu hakitakufunga, lakini kwa vyovyote vile usimrudishe mwanangu huko.”
9 Basi, mtumishi huyo akaweka mkono wake mapajani mwa Abrahamu, bwana wake, akaapa kuhusu jambo hilo.