25 Wa kwanza alikuwa mwekundu, mwenye nywele mwili wote; hivyo wakamwita Esau.
26 Wa pili alizaliwa akiwa amemshika Esau kisigino, hivyo wakampa jina Yakobo. Isaka alikuwa na umri wa miaka sitini wakati Esau na Yakobo walipozaliwa.
27 Watoto hao wakakua; Esau akawa mwindaji hodari, mpenda maisha ya mbugani, na Yakobo akawa mtu mtulivu, mpenda maisha ya nyumbani.
28 Basi, Isaka akampenda Esau kwa sababu alipenda kula mawindo yake, lakini Rebeka akampenda Yakobo.
29 Siku moja, Yakobo alipokuwa anapika dengu, Esau alirudi nyumbani kutoka mawindoni ana njaa sana.
30 Kwa hiyo akamwambia Yakobo, “Nafa njaa; tafadhali, nigawie chakula hicho chekundu nile.” (Ndiyo maana walimpanga jina Edomu yaani mwekundu).
31 Yakobo akajibu, “Kwanza niuzie haki yako ya mzaliwa wa kwanza.”