1 Basi, Yosefu akaenda kwa Farao, akamwambia, “Baba yangu na ndugu zangu pamoja na kondoo, ng'ombe na mali yao yote, wamefika kutoka nchi ya Kanaani. Sasa wako katika eneo la Gosheni.”
2 Yosefu alikuwa amewachukua ndugu zake watano, akawajulisha kwa Farao.
3 Farao akawauliza, “Kazi yenu ni nini?” Wakamjibu, “Bwana, sisi watumishi wako ni wachungaji, kama walivyokuwa babu zetu.”
4 Kisha wakamwambia Farao, “Sisi watumishi wako tumekuja kukaa kama wageni humu nchini kwa kuwa njaa ni kali huko Kanaani na hakuna tena malisho kwa mifugo yetu. Hivyo, bwana, tunakuomba, sisi watumishi wako, uturuhusu kukaa katika eneo la Gosheni.”
5 Farao akamwambia Yosefu, “Baba yako na ndugu zako wamekujia wewe.
6 Nchi yote ya Misri iko chini yako; wape baba yako na ndugu zako sehemu bora ya nchi hii. Waache wakae katika eneo la Gosheni. Na iwapo unawafahamu watu stadi miongoni mwao, wateue wawe waangalizi wa mifugo yangu.”
7 Kisha, Yosefu akamleta baba yake Yakobo kumwamkia Farao; naye Yakobo akampa Farao baraka zake.