8 Baraki akamwambia Debora, “Kama utakwenda pamoja nami, nitakwenda. Lakini usipokwenda pamoja nami, sitakwenda.”
9 Debora akamjibu, “Sawa. Nitakwenda pamoja nawe; lakini hutapata heshima yoyote ya ushindi, maana Mwenyezi-Mungu, atamtia Sisera mikononi mwa mwanamke.” Basi, Debora akafuatana na Baraki kwenda Kedeshi.
10 Baraki akayaita makabila ya Naftali na Zebuluni huko Kedeshi; watu 10,000 wakamfuata. Debora akaenda pamoja naye.
11 Wakati huo, Heberi, Mkeni, alikuwa amejitenga na Wakeni wenzake ambao ni wazawa wa Hobabu, baba mkwe wa Mose. Alikuwa amepiga hema lake mbali huko kwenye mwaloni wa Zaananimu, karibu na Kedeshi.
12 Sisera alipopata habari kwamba Baraki mwana wa Abinoamu amekwenda mlimani Tabori,
13 alikusanya jeshi lake lote na magari yake mia tisa ya chuma, akaondoka Harosheth-hagoimu, akaenda kwenye mto Kishoni.
14 Debora akamwambia Baraki, “Inuka! Leo ni siku ambayo Mwenyezi-Mungu atamtia Sisera mikononi mwako. Mwenyezi-Mungu anakwenda mbele yako.” Basi, Baraki akashuka kutoka mlimani Tabori akiwaongoza watu wake 10,000.