15 Wakazikataa sheria zake, na agano lake, alilolifanya na baba zao; na shuhuda zake alizowashuhudia; wakafuata ubatili, wakawa ubatili, nao wakaandamana na mataifa waliowazunguka, ambao BWANA alikuwa amewaagiza, wasitende kwa mfano wao.
16 Wakaziacha amri zote za BWANA, Mungu wao, wakajifanyizia sanamu za kusubu, yaani, ndama mbili, wakafanya na Ashera, wakaliabudu jeshi lote la mbinguni, wakamtumikia Baali.
17 Wakawapitisha watoto wao, waume na wake, motoni, wakapiga ramli, wakafanya uchawi, wakajiuza nafsi zao wapate kufanya yaliyo maovu machoni pa BWANA, hata kumkasirisha.
18 Kwa hiyo BWANA akawaghadhibikia Israeli sana, akawahamisha mbali na uso wake; wala hapana aliyesalia ila kabila ya Yuda peke yake.
19 Hata na watu wa Yuda hawakuyashika maagizo ya BWANA, Mungu wao, lakini walikwenda katika amri za Israeli walizokuwa wamezifanya wenyewe.
20 Basi BWANA akakikataa kizazi chote cha Israeli, akawatesa, na kuwatia katika mikono ya watu wenye kuwateka nyara, hata alipokwisha kuwatupa, watoke machoni pake.
21 Maana aliwatenga mbali Israeli na nyumba ya Daudi; nao wakamfanya Yeroboamu mwana wa Nebati kuwa mfalme; Yeroboamu akawavuta Israeli wasimfuate BWANA, akawakosesha kosa kubwa.