14 Kwa hiyo akapeleka huko farasi, na magari, na jeshi kubwa; wakafika usiku, wakauzingira mji ule pande zote.
15 Hata asubuhi na mapema mtumishi wake yule mtu wa Mungu alipoondoka, na kwenda nje, kumbe! Pana jeshi la watu, na farasi na magari, wameuzingira mji ule. Mtumishi wake akamwambia, Ole wetu! Bwana wangu, tufanyeje?
16 Akamjibu, Usiogope; maana walio pamoja nasi ni wengi kuliko wale walio pamoja nao.
17 Elisha akaomba, akasema, Ee BWANA, nakusihi, mfumbue macho yake, apate kuona. BWANA akamfumbua macho yule mtumishi; naye akaona; na tazama, kile kilima kilikuwa kimejaa farasi na magari ya moto yaliyomzunguka Elisha pande zote.
18 Na walipomtelemkia Elisha akamwomba BWANA, akasema, Uwapige, nakusihi, watu hawa kwa upofu. Akawapiga kwa upofu sawasawa na neno la Elisha.
19 Elisha akawaambia, Njia hii siyo, na mji huu sio, nifuateni mimi, nami nitawapeleka kwa mtu yule mnayemtafuta. Akawapeleka Samaria.
20 Hata walipokwisha kuingia Samaria, Elisha akasema, BWANA wafumbue macho watu hawa, wapate kuona. BWANA akawafumbua macho wakaona; kumbe! Walikuwa katikati ya Samaria.