19 Elisha akawaambia, Njia hii siyo, na mji huu sio, nifuateni mimi, nami nitawapeleka kwa mtu yule mnayemtafuta. Akawapeleka Samaria.
20 Hata walipokwisha kuingia Samaria, Elisha akasema, BWANA wafumbue macho watu hawa, wapate kuona. BWANA akawafumbua macho wakaona; kumbe! Walikuwa katikati ya Samaria.
21 Naye mfalme wa Israeli alipowaona, akamwambia Elisha, Ee baba yangu, niwapige? Niwapige?
22 Akamjibu, Usiwapige; je! Ungetaka kuwapiga watu ambao umewatwaa mateka kwa upanga wako na uta wako? Weka chakula na maji mbele yao, wapate kula na kunywa, na kwenda kwa bwana wao.
23 Basi akawaandalia chakula tele; nao walipokwisha kula na kunywa, akawaacha, wakaenda zao kwa bwana wao. Na vikosi vya Shamu havikuja tena katika nchi ya Israeli.
24 Ikawa baada ya hayo, Ben-hadadi mfalme wa Shamu akakusanya majeshi yake yote, akakwea akauhusuru Samaria.
25 Njaa ikawa kuu huko Samaria; na tazama, wakauhusuru, hata kichwa cha punda kikapata kuuzwa kwa vipande themanini vya fedha, na kibaba cha mavi ya njiwa kwa vipande vitano vya fedha.