24 Ng’ombe pia na wana-punda wailimao nchi watakula chakula kilichokolea, kilichopepetwa kwa ungo na kwa pepeo.
25 Na juu ya kila mlima mrefu, na juu ya kila kilima kilichoinuka, itakuwapo mito na vijito vya maji, katika siku ya machinjo makuu itakapoanguka minara.
26 Na tena nuru ya mwezi itakuwa kama nuru ya jua, na nuru ya jua itaongezeka mara saba, kama nuru ya siku saba, katika siku ile BWANA atakapofunga mapigo ya watu wake, na kuliponya pigo la jeraha yao.
27 Tazama, jina la BWANA linakuja kutoka mbali sana, linawaka kwa hasira yake, kwa moshi mwingi sana unaopaa juu; midomo yake imejaa ghadhabu, na ulimi wake ni moto ulao;
28 na pumzi yake ni kijito kifurikacho, kifikacho hata shingoni, kupepeta mataifa kwa ungo wa ubatili; na lijamu ikoseshayo itakuwa katika taya za watu.
29 Mtakuwa na wimbo kama vile wakati wa usiku, ishikwapo sikukuu takatifu, mtakuwa na furaha ya moyo kama vile mtu aendapo na filimbi katika mlima wa BWANA, aliye Mwamba wa Israeli.
30 Naye BWANA atawasikizisha watu sauti yake ya utukufu, naye atawaonyesha jinsi mkono wake ushukavyo, na ghadhabu ya hasira yake, na mwako wa moto ulao, pamoja na dhoruba, na tufani, na mvua ya mawe ya barafu.