13 Kisha yule amiri akasimama akalia kwa sauti kuu kwa lugha ya Kiyahudi, akisema, Lisikieni neno la mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru.
14 Mfalme asema hivi; Hezekia asiwadanganye, kwa maana hataweza kuwaokoa;
15 wala msimwache Hezekia kuwatia moyo wa kumtumaini BWANA; akisema, BWANA bila shaka atatuokoa, mji huu hautatiwa katika mkono wa mfalme wa Ashuru.
16 Msimsikilize Hezekia; maana mfalme wa Ashuru asema hivi, Fanyeni suluhu na mimi, mkatoke mnijie, mkale kila mtu matunda ya mzabibu wake na matunda ya mtini wake, mkanywe kila mmoja maji ya birika yake mwenyewe;
17 hata nije nikawachukue mpaka nchi iliyo kama nchi yenu wenyewe, nchi ya nafaka na divai, nchi ya mkate na mashamba ya mizabibu.
18 Jihadharini, asije Hezekia akawadanganya, akisema, BWANA atatuokoa. Je! Yuko mungu mmoja wa mataifa aliyewaokoa watu wake na mkono wa mfalme wa Ashuru?
19 Wako wapi miungu ya Hamathi na ya Arpadi? Wako wapi miungu ya Sefarvaimu? Je! Wameiokoa Samaria na mkono wangu?