1 Kwa ajili ya Sayuni sitanyamaza, na kwa ajili ya Yerusalemu sitatulia, hata haki yake itakapotokea kama mwangaza, na wokovu wake kama taa iwakayo.
2 Na mataifa wataiona haki yako, na wafalme wote watauona utukufu wako; nawe utaitwa jina jipya, litakalotajwa na kinywa cha BWANA.
3 Nawe utakuwa taji ya uzuri katika mkono wa BWANA, na kilemba cha kifalme mkononi mwa Mungu wako.
4 Hutaitwa tena Aliyeachwa, wala nchi yako haitaitwa tena, Ukiwa; bali utaitwa Hefsiba; na nchi yako Beula; kwa kuwa BWANA anakufurahia, na nchi yako itaolewa.