Mit. 12 SUV

1 Kila apendaye mafundisho hupenda maarifa;Bali yeye achukiaye kulaumiwa ni kama mnyama.

2 Mtu mwema atapata upendeleo kwa BWANA;Bali mtu wa hila atahukumiwa naye.

3 Mtu hatathibitika kwa njia ya uovu;Shina la mwenye haki halitaondolewa kamwe.

4 Mwanamke mwema ni taji ya mumewe;Bali aaibishaye ni kama kuoza mifupani mwake.

5 Mawazo ya mwenye haki ni adili;Bali mashauri ya mtu mwovu ni hadaa.

6 Maneno ya waovu huotea damu;Bali kinywa cha wanyofu kitawaokoa.

7 Waovu huangamia, hata hawako tena;Bali nyumba ya mwenye haki itasimama.

8 Mtu atasifiwa kwa kadiri ya akili zake;Bali mwenye moyo wa ukaidi atadharauliwa.

9 Afadhali mtu anayedharauliwa, ikiwa ana mtumwa,Kuliko ajisifuye, ikiwa anahitaji chakula.

10 Mwenye haki huufikiri uhai wa mnyama wake;Bali huruma za mtu mwovu ni ukatili.

11 Alimaye shamba lake atakuwa na chakula tele;Bali afuataye mambo ya upuzi hana ufahamu.

12 Asiye haki hutamani nyavu za wabaya;Bali shina lao wenye haki huleta matunda.

13 Katika kosa la midomo kuna mtego kwa mbaya;Bali mwenye haki atatoka katika taabu.

14 Mtu atashiba mema kwa matunda ya kinywa chake;Na atarudishiwa matendo ya mikono yake.

15 Njia ya mpumbavu imenyoka machoni pake mwenyewe;Bali yeye aliye na hekima husikiliza shauri.

16 Ghadhabu ya mpumbavu hujulika mara;Bali mtu mwerevu husitiri aibu.

17 Atamkaye maneno ya kweli hufunua haki;Bali shahidi wa uongo hutamka hila.

18 Kuna anenaye bila kufikiri, kama kuchoma kwa upanga;Bali ulimi wa mwenye haki ni afya.

19 Mdomo wa kweli utathibitishwa milele;Bali ulimi wa uongo ni wa kitambo tu.

20 Hila imo mioyoni mwao wafikirio uovu;Bali wafanyao mashauri ya amani, kwao kuna furaha.

21 Mwenye haki hatapatikana na msiba wo wote;Bali wasio haki watajazwa mabaya.

22 Midomo ya uongo ni chukizo kwa BWANA;Bali watendao uaminifu ndio furaha yake.

23 Mwanadamu mwenye busara husitiri maarifa;Bali moyo wa wapumbavu hutangaza upumbavu.

24 Mkono wa mwenye bidii utatawala;Bali mvivu atalipishwa kodi.

25 Uzito katika moyo wa mtu huuinamisha;Bali neno jema huufurahisha.

26 Mwenye haki ni kiongozi cha mwenzake;Bali njia ya wasio haki huwakosesha.

27 Mtu mvivu hapiki mawindo yake;Bali mwenye bidii anazo mali za thamani.

Sura

1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13 14 15 16 17 18 19 20 21 22 23 24 25 26 27 28 29 30 31