Mit. 15 SUV

1 Jawabu la upole hugeuza hasira;Bali neno liumizalo huchochea ghadhabu.

2 Ulimi wa mwenye hekima hutamka maarifa vizuri;Bali vinywa vya wapumbavu humwaga upumbavu.

3 Macho ya BWANA yako kila mahali;Yakimchunguza mbaya na mwema.

4 Ulimi safi ni mti wa uzima;Bali ukorofi wa ulimi huvunja moyo.

5 Mpumbavu hudharau kurudiwa na babaye;Bali yeye aangaliaye maonyo hupata busara.

6 Katika nyumba ya mwenye haki mna akiba nyingi;Bali mapato ya mtu mbaya huwa taabu tu.

7 Midomo ya mwenye haki hueneza maarifa;Bali moyo wa mpumbavu haufanyi hivyo.

8 Sadaka ya mtu mbaya ni chukizo kwa BWANA;Bali maombi ya mtu mnyofu ni furaha yake.

9 Njia ya mtu mbaya ni chukizo kwa BWANA;Bali humpenda mtu afuatiaye wema.

10 Adhabu kali ina yeye aiachaye njia;Naye achukiaye kukemewa atakufa.

11 Kuzimu na Uharibifu vi wazi mbele za BWANA;Si zaidi basi, mioyo ya wanadamu?

12 Mwenye mzaha hapendi kukaripiwa;Wala yeye hawaendei wenye hekima.

13 Moyo wa furaha huchangamsha uso;Bali kwa huzuni ya moyo roho hupondeka.

14 Moyo wa mwenye ufahamu hutafuta maarifa;Bali kinywa cha wapumbavu hula upumbavu.

15 Siku zote za mtu ateswaye ni mbaya;Bali ukunjufu wa moyo ni karamu ya daima.

16 Kuwa na mali chache pamoja na kumcha BWANA;Ni bora kuliko mali nyingi pamoja na taabu.

17 Chakula cha mboga penye mapendano;Ni bora kuliko ng’ombe aliyenona pamoja na kuchukiana.

18 Mtu wa hasira huchochea ugomvi;Bali asiye mwepesi wa hasira hutuliza mashindano.

19 Njia ya mtu mvivu ni kama boma la miiba;Bali mapito yao wenye unyofu hufanyika njia kuu.

20 Mwana mwenye hekima humfurahisha babaye;Bali mpumbavu humdharau mamaye.

21 Upumbavu ni furaha kwake aliyepungukiwa na akili;Bali mwenye ufahamu huunyosha mwenendo wake.

22 Pasipo mashauri makusudi hubatilika;Bali kwa wingi wa washauri huthibithika.

23 Mtu hulifurahia jibu la kinywa chake;Na neno linenwalo wakati wa kufaa ni jema kama nini!

24 Kwa mtu mwenye akili njia ya uhai huenda juu;Ili atoke katika kuzimu chini.

25 BWANA ataing’oa nyumba ya mwenye kiburi;Bali atauthibitisha mpaka wa mjane.

26 Mashauri mabaya ni chukizo kwa BWANA;Bali maneno yapendezayo ni safi.

27 Atamaniye faida huifadhaisha nyumba yake mwenyewe;Bali achukiaye zawadi ataishi.

28 Moyo wa mwenye haki hufikiri jinsi atakavyojibu;Bali kinywa cha wasio haki humwaga mabaya.

29 BWANA yu mbali na wasio haki;Bali huisikia sala ya mwenye haki.

30 Mng’ao wa macho huufurahisha moyo;Habari njema huinenepesha mifupa.

31 Sikio lisikilizalo lawama yenye uhaiLitakaa kati yao wenye hekima.

32 Akataaye maonyo huidharau nafsi yake mwenyewe;Bali yeye asikilizaye lawama hujipatia ufahamu.

Sura

1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13 14 15 16 17 18 19 20 21 22 23 24 25 26 27 28 29 30 31